29 Dec

WAKAZI wa mkoa wa Simiyu wametakiwa kuachana na mila potofu katika mapambano ya ugonjwa kipindupindu ambapo kwa sasa ugonjwa huo wa mlipuko umekuwa ukisumbua katika baadhi ya maeneo ya mkoani hapo.

Rai hiyo imetolewa jana na Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi wakati wa maombi malumu na matembezi ya upendo wa kuombea mkoa huo pamoja na Taifa kwa ujumla.

Amesema baadhi ya mila zinazoleta changamoto ni kama mila potofu ya Baba mkwe na mama mkwe kutumia choo cha pamoja.

Akielezea zaidi, Kihongosi amesema wananchi wa mkoa huo waachane na dhana kuwa maji maji yaliotibiwa na Wakala wa Usambazaji wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA)mkoa wa Simiyu kuwa maji hayo hayafai.

‘’Maji yaliotibiwa na RUWASA, ni mazuri na yamewekewa dawa zilizopitishwa na watalaam wetu kutoka Wizara ya Afya’’ amesema.

Kihongosi amewataka pia wakazi hao wa mkoa wa Simiyu kuachana na dhana kuwa maji yaliotibiwa yanapunguza nguvu za kiume pamoja na kuleta madhara katika kizazi.

‘’Naishukuru Wizara ya Afya ya kuleta kampeni ya Mtu Ni Afya katika kuweza kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa kipindupindu katika mkoa wetu. Tunatambua mkoa wetu unachangamoto ya kipindupindu, awali tulikuwa na idadi kubwa sana ya watu waliopata maambukizi ya ugonjwa huu’’ amesema.

Katika hatua nyingine, Kihongosi amewataka wakazi wa mkoa wa Simiyu kuchemsha maji pamoja kuwa na matumizi ya vyoo bora.

‘’Mimi kama mkuu wa mkoa wa Simiyu, tumetembelea kata zote 133 ndani ya mkoa huu kwa kutoa elimu kwa wananchi na kuelezea madhara ya kipindupindu na jitihada hizo zilisaidia katika namna kubwa ya kupunguza madhara ya kipindupindu’’ amesema.